Tuesday, December 30, 2008

MKOJO WA KONDOO HUHIFADHI MBEGU ZA MAHINDI

Na.Mwantumu Jongo.
Mbegu za mahindi huhifadhiwa ili zisiharibiwe na wadudu kwa kumwagiwa mkojo wa kondoo .Kuna njia nyingi za kuhifadhi mazao yetu lakini wasukuma wamenitolea kali ya mwaka kwani wao wanahifadhi mbegu zao za mahindi kwa namna ya pekee tumezoea kuona mbegu hii zikihifadhiwa kwa kufungwa mahindi pamoja na majani yake na kuhifadhiwa juu ya dali la jiko ili ziweze kukaushwa na moshi wa jikoni.

Lakini katika eneo la Kitangili lililopo karibu na stesheni ya reli mjini shinyanga ndipo nilipokutana na uvumbuzi wa aina yake kwani bwana Kulwa Steven alisema tangu utoto wao huhifadhi mbegu za mahindi kwa kutumia njia hii .

Ambapo mkulima hutayarisha “jeka”ni sehemu ya kuhifadhia mbegu kama vile ilivyo mtungi .Kuna njia mbili za kujenga jeka,mahitaji yake ni kamba ,miti mirefu na mifupi na mabua.Katika njia ya kwanza mkulima hutafuta miti mirefu , na nguzo fupi anachimbia chini ya ardhi ,kisha analaza fito mstari mmoja halafu zile mbegu za mahindi anazifunga kwa kuyaunganisha majani ya yale mahindi yenyewe kwa yenyewe na kuanza kuyapanga kwenye fito njia hii kwa kisukuma huitwa nshijite .

Njia ya pili ni ile Mkulima hutafuta miti mirefu na mifupi anatengeneza kichanja halafu pembeni anasimamisha miti mirefu halafu anasiliba na mabua unaweza ukatengeneza kajumba kwa juu ili kuzikinga mbegu zako katika kipindi cha kiangazi .

Mkulima huchukua mahindi mabichi hayatoi majani yake unayaunganisha na kuyafunga pamoja kisha unayahifadhi kwenye jeka lake .Vijana hutumwa kuleta mkojo wa kondoo ambao hupatikana kwa kumshika kondoo na mwengine hukinga ule mkojo inasemekana kondoo ni nadra kukojoa lakini akishikwa hukojoa haraka na kumwagia katika jeka lenye mbegu za mahindi .Mbegu za mahindi huweza kuhifadhiwa kwa njia hii kwa muda wa mwaka mmoja na zaidi bila kuharibiwa na wadudu.

Bwana Steven anaamini wadudu hawapendi harufu ya mikojo ya kondoo hivyo wakikaribia katika jeka huondoka mara moja na kuziweka mbegu zao katika hali ya usalama .
Kwa upande wangu nimebahatika kuona njia nyingi za kuhifadhi mbegu za mahindi kama vile kuhifadhi katika mti wenye njia panda unalaza mti na kuyafunga mahindi yako nji hii na nyinginezo hutumika sana katika vijiji vingi nchini Tanzania hivyo hatuna budi kuzitumia ili tuweze kuwa na uhakika wa kuhifadhi mbegu za mahindi.
Serikali na taasisi binafsi ziziendeleze njia hizi za asili kwa kufanyia utafiti ili kuwa na uhakika zaidi wa ubora wa njia hizi kwani tukumbuke kuna usemi usemao kuwa ya kale ni dhahabu.

No comments: