Wednesday, November 19, 2008

UMWAGILIAJI KWA NJIA YA MATONE WATEKELEZWA SHINYANGA

Na.Mwantumu Jongo
Wakulima wa kikundi cha nguvu kazi kilichopo katika kijiji cha Mwagala mkoa wa Shinyanga wamefadhiliwa na shirika la chakula duniani(FAO) kupitia JICA mradi wa umwagiliaji kwa njia ya matone wenye thamani ya shilingi milioni 3.4 unaoendeshwa katika vijiji vya chibe na Heregani.Mradi huu umewapatia ajira wanawake 30 na wanaume 30 ambao hapo awali walikuwa wakihangaika katika kutafuta njia sahihi ya kupambana na uhaba wa maji.

Umwagiliaji kwa njia ya matone ni teknolojia mpya ya ya kilimo cha umwagiliajia kwa kutumia maji kidogo na kuzalisha mboga za kutosha wakati wa kingazi . Teknolojia hii ya umwagiliaji kwa njia ya matone hutumika kwenye nchi ambazo hukabiliwa na ukame kwa muda mrefu na hutumia ndoo ,debe,au chombo chochote kinachoweza kuchukua maji ya kutosha na kinatobolewa ili kuweka mipira maalum ya kuwezesha maji kutiririka hadi kwenye mche au mimea uliopo bustanini.

Teknolojia hii mpya ilianzishawa huko marekani na Israeli na imekuwa ikiwanufaisha wakulima wadogo wadogo kwa kuwawezesha kupata mboga za kutosha kipindi cha kiangazi.Kilimo cha umwagiliaji bustani kwa njia ya matone kimeanza kutumika na kukubalika kwa wakulima katika nchi kame 26 za bara la afrika zikiwemo Kenya na Tanzania.

Bwana A.A.chuwa afisa kilimo wa manispaa ya shinyanga aliweza kuhudhuria mafunzo yaliyotolewa na afisa mshirikishaji wa shirika la mtandao wa habari za nyanda kame ALIN (Arid land information nertwork) bwana Noah Lusaka alisema katika majaribio yaliyofanywa DONET (miyuji ,msalato,matumbulu,na nzuguni baadhi ya wananchi wameridhika kuwa teknolojia hii inaweza kuwapatia mboga za kutosha .

Hali hii ikawafanya maafisa hawa wa kilimo watekeleze kwa vitendo mafunzo haya katika eneo lao kwani faida za teknolojia hii ni kuwa kazi ya umwagiliiaji inaweza kufanywa na mtu yeyote kwa kujaza maji kwenye ndoo au mwenye shamba kufanya hivyo na kuendelea na kazi zingine bustani.

Hata hivyo bwana Edger Muzio bwana shamba wa Mwagala yeye alipopata mafunzo haya alipigania kwa dhati watu wake waweze kunufaika na mradi huo na hatimaye hizi ndizo juhudi zake kwani amefanikiwa kuuleta mradi katika eneo lake naye anawashauri watu wake watumie njia ya umwagiliaji bustani kwa matone kwani bustani haziwi na magugu au majani yanayohitajika kupaliliwa kwa kuwa maji hulenga kwenye mche na hivyo kusababisha majani yasiyohitajika yasiote .

Aidha magonjwa yanayoshambualia mboga au miche ni machache kwa kuwa maji hayarushi vumbi kama yanavyomwagiliwa kwa kutumia ndoo ,debe au mipira ya kawaida na utayarishaji wa umwagiliaji huo unahitaji ndoo,debe au chombo kingine ambacho huwekwa kwenye eneo lililoinuka ili mipira inapofungwa kwenye chombo chenye maji iweze kutiririrsha maji kwa urahisi hadi kwenye mimea inayotakiwa kunyeshewa .

Alisema ni vizuri mipira ya kumwagilia ikawa na na vifaa vya kuhakikisha mipira hiyo haipeperushi na upepo na kama mwenye bustani anahisi wezi wanaweza wakaiba vifaa hivyo ni vyema avihifadhi ndani wakati wa usiku na nyakati za mvua .

Pia wakati wa palizi ni vizuri mwenye bustani au anayefanya kazi hiyo awe mwangalifu ili asikate mipira ya kumwagilia licha ya hayo kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia teknolojia hii kitafanikiwa zaidi kama bustani itakuwa kwenye eneo la tambarare na ambalo halina mabonde au mzunguko iwapo bustani itakuwa na mabonde au mizunguko maji hayatoki mengi kama yanavyotazamiwa .

Njia hii ya umwagiliaji bustani kwa matone hutumia viungio washa ya mpira ,kichujio,vibanio viwili ,vipande vya mipira ,mipira miwili kila mmoja wenye urefu wa futi 50 na kisha mkulima atatoboa tundu moja lenye kipenyo cha inchi moja(1) kwenye kitako cha ndoo au pipa na kupachika washa pampu kwenye tundu la ndoo na kuweka kiungio cha ndani kwenye washa na halafu ataweka kiungio cha nje ili vibanane .

Baada ya kufanya hivyo mkulima atapachika vile vipande viwili vya mipira ya kumwagilia maji chini ya kichujio na ataisukuma iingie kwenye kiungo cha nje na iweke mipira ya kumwagilia .Maji yanapoanza kutiririka kwenye mipira ya kumwagilia acha kwa muda kidogo ndipo uhakikishe mwisho ni mwa mipira hiyo panafungwa kwa kuikunja kidogo na kuweka kibanio ili maji yasitoke nje bali yaanze kutoka kwenye matundu ya kumwagilia.

Hakikisha tundu linalotoa maji linalenga kwenye mmea au mche unaotaka upate maji ni vizuri bustani iwe na majani yaliyosambazwa juu yake ili kuhakikisha unyevu unabaki bustanini.Lazima maji yanayotumika kumwagilia yawe hayana mchanga au uchafu wowote ambao unaweza kuzuia maji yasitoke kwenye matundu.

Licha ya hayo wakulima wa bustani za mbogamboga hawajapata elimu ya ujasiliamali kutokuwa na misingi ya kutosha kuweza kuwekeza katika bustani hizo kwani wana hitaji mikopo ili waweze kujipatia rasilimali endelevu .

Wakati sasa umefika kwa wadau mbalimbali kuunga mkono kwa vitendo utekelezaji uliofanywa na wenzetu wa mkoa wa Shinyanga kwani wao wameweza kuhamasisha jamii yao kuweza kutekeleza umwagiliaji bustani kwa matone kwa vitendo tuwaunge mkono kwa njia mbalimbali hata kwa kuwapa mafunzo na ushauri katika nini cha kufanya ili waweze kupiga hatua katika safari yao waliyoianza.

No comments: