Tuesday, December 30, 2008

UVUNAJI WA MAJI KWA NJIA YA MAJALUBA

Na.Mwantumu Jongo.
Kitangili ni eneo linalopatikana katika wilaya ya Shinyanga mjini baadhi ya wakazi wake wanalima mpunga kwa kutumia mitaro badala ya maji ya mvua kumwagika ovyo yanaelekewa kwenye mashamba maarufu kama majaluba.Majaluba ni sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kupanda mpunga.Njia hii husaidia sana katika kuhifadhi maji hususani katika maeneo ya nyanda kame ili kuweza kuongeza uzalishaji katika eneo dogo.

Upatikanaji wa maji katika majaruba unafanyika kwa kutengeneza mitaro inayotiririsha maji na kuielekeza kwenye majaruba. Utengenezaji mitaro unahitaji ushirikiano hasa pale kunapokuwa na majaruba mengi yanayomilikiwa na wakulima mbalimbali.

Hivyo mitaro hii hutengenezwa na wakulima kwa kuyaelekeza maji ya mvua katika majaruba yao. Njia hii imekuwa na manufaa sana kwani hakuna maji yanayoachwa ovyo. Kwa hiyo hii ni namna mojawapo ya utumiaji mzuri wa maji.

Hali hii imewafanya wakulima wengi kupanua mavuno yao. Awali mkulima alingoja mvua tu huku miteremko ya maji ikitiririsha maji ovyo. Baada ya ugunduzi huu wa taaluma hii, wakulima wamejikuta wakinufaika sana. Sasa hivi wakulima wamenzisha vikundi vya kutengeneza mitaro ya namna hii katika azma ya kuboresha kilimo cha mpunga.


UTAYASHAJI WA JARUBA
Unalima na kuweka kingo nne za matuta baada ya siku saba unayachanganya majani yaliooza na udongo ni mbolea. Majani yasiyooza unayalundika pembeni ya shamba ili yasiote huchanganywa na udongo baada ya mavuno hutumika kama mbolea. Unaangalia uelekeo wa maji ardhi iwe sawa ukiona kilima unashushia kwenye bonde hii inasaidia kutunza maji kwani mpunga unahitaji maji mengi.Hakikisha miche ya mpunga haizami kwenye maji .

KUOTESHA MBEGU
Kipindi cha mwezi wa kumi mkulima huotesha mbegu kwa ajili ya kilimo cha mpunga kuna njia mbili za kuotesha mbegu njia ya kwanza ni ile ya kulima kitalu pembeni ya jaluba sehemu yenye unyevu nyevu na kuotesha mbegu zikiota miche ikikuwa ndipo huhamishwa na kupanda kwenye majaluba yaliyoandaliwa .
Aina ya pili ni kutifua jaluba na unamwaga mbegu za mpunga ndani ya jaluba zima kwa kusubiri mvua ili mbegu iote.

UPANDAJI
Miche ikikuwa unangoa na kupanda katika jaluba katika njia ya pili kama imeota miche imeota mingi unahamisha na kupanda katika jaluba jingine eneo likiwa na rutuba nyingi unapanda mche mmoja.Majaluba yan milango ya kupokea maji na kutoa mfano mpunga ukianza kucahnua unahitaji maji hivyo milango yake huwa wazi ili kuingiza maji kwenye jaluba.
UPALILIAJI
Kwenye jaluba kukiwa na maji ya kutosha majani yanakufa kwa kuoza katika maji ardhi inakuwa laini mkulima huyangoa na mkono lakini unatakiwa uchukue tahadhari kwani majani ya mpunga yanafanana na magugu hivyo unashauriwa usubiri hadi miche ifikie inchi kumu na tano(15).
UVUNAJI
Baada ya takriban miezi mitatu, uvunaji wa mpunga huanza. Uvunaji uko katika njia mbili nazo ni (a) uvunaji wa kutumia kisu kwa kukata kila kikonyo cha mpunga (b) uvunaji wa kutumia kiberenge yaani kukata shina lote la mpunga kwa kukusanya katika makundi makundi.
Kisha unaandaa sehemu safi ambayo itakuwa haina mchanga. Eneo hili utatumia jembe kuondoa nyasi na mchanga. Fagia eneo lako kwa kuondoa mchanga. Pale inapobidi, unaweza kutumia mavi mabichi ya ng’ombe kwa kuyafanya yawe mazito kiasi. Changanya katika ndoo hakikisha hakuna mabonge mabonge ya mavi ya ng’ombe.
Chukua mfagio mgumu wa nje na kumwaga huo mkorogo wa mavi ya ng’ombe. Fagia mkrogo huo na kuacha mwingine unate sehemu uliyoandaa. Ukisha kamilisha acha pakauke. Unaweza ukapaacha pakauke kwa muda wa masaa mawili au matatu na kuanza kazi.
Somba mpunga wote uliokata na kuurundika katika eneo uliloandaa kwa ajili ya kupigia. Daima unapoleta panga katika mstari katika duara kwa kurundika ukiacha nafasi kigodo katikati. Anza kuchukua kiasi unachoweza kukiwebeba mikononi na kukiinua juu kisha kipigize sehemu uliyoacha wazi. Pigiza mara tatu au nne kutegemea hakuna mpunga unaosali kwenye majani ya mpunga. Endelea hadi rundo lako limekwisha.

Kama kuna mpunga mwingine, endelea kufanya hivi mpaka umalize. Ukiona umechoka, unaweza kuamua kupeta mpunga uliopiga kwa kutumia ndoo. Chota mpunga kadri unavyoweza kubeba na kuinua juu pembeni kidogo mwa mpunga uliopiga. Mwaga kidogo kidogo utaona pumba na uchafu mwingine unapeperushwa na upepo.na hivyo mpunga safi kubaki karibu na miguu yako. Endelea mpaka umalize rundo la mpunga uliopiga.
Kazi itakayofuata ni kuweka katika mifuko unashona na kusafirisha nyumbani.Kazi ya uvunaji itakuwa imekamilika.
Uvunaji wa kukata kila kikonyo cha mpunga unafanyika kwa uchache sana kwani unapoteza wakati mno na pia nguvu nyingi. Mpunga unapokuwa umevunwa, huwekwa ndani kwa muda wa mwezi mmoja au miezi miwili ili ukauke vilivyo. Hatimaye eneo maalum la kupigia kama nililolieleza hapo juu huandaliwa. Mpunga hutolewa nje na kuachwa kwa muda mfupi ukauke. Kazi inayofuata ni kupiga mpunga kwa kutumia fimbo ndogo ndogo. Upigaji huu ni wa kuhakikisha kuwa hakuna mpunga unasalia kwenye vikonyo vyote.
Kazi ya kupeta inafuata baada ya kumaliza kupiga. Baada ya kupeta mpunga hujazwa katika magunia ama huwekwa katika ghala.

MAFANIKIO
Mavuno mengi katika eneo dogo.
Shamba kuwa na rutuba
Kukiwa na maji ya kutosha kama kukiingiliana na mto kuna uwezekano mkubwa wa kupata samaki.

MATATIZO
Wadudu waitwao ngegeshi hupatikana wakati maji yakiwa yamepungua hukata majani ya mpunga.
Ndege ambao kwa sasa hutumia njia za kienyeji kuwa fukuza kama kuchonga masanamu yanayofananna na watu,kanda za redio hufungwa pembeni mwa kingona hata mabetri hubondwa na lie bati lake kwa vie tu lina mngao huwakimbiza ndege.

1 comment:

Bennet said...

Tumia CD (compact disc) ambazo zimeharibika kwa kusining'iniza kwenye kamba, mng'ao wake huweza kufukuza ndege wengi hata kunguru pia