Tuesday, December 30, 2008

SUNGUSUNGU WATUNZA MAZINGIRA

Na.Mwantumu Jongo.
Wengi wetu tumekuwa tukifahamu kuwa sungusungu ni jina la wadudu wadogo wadogo weusi ambao hutambaa ardhini.Wadudu hawa huuma pindi wanapokandamizwa.Mtu aumwapo na wadudu hawa huisi uchungu. Neno hili lilipendekezwa litumike kwa kikundi hicho cha Usalama kwa sababu ya kujihami kwao kwa haraka wawapo na tatizo.
Licha ya kwamba sungusungu hawa adhabu zao haziendani na sheria ya nchi mfano mzuri aliyetengwa haruhusiwi katika kufanya ibada lakini wana mchango mkubwa katika kutunza mazingira yetu.

“Kutunza mazingira ni sehemu ya kazi yao “alisema bwana W.C.Mlenge.
NAFRAC ilipoanza mradi ilikuta sungusungu imeshatawazwa . Mnamo mwaka 1992 mwezi wa saba walienda Bariadi kufanya utafiti wa taasisi za kiasili zitasaidiaje katika kutunza mazingira wakaitisha mkutano wakiongozwa na chifu wao wa zamani ambaye alijua mambo ya mila na uhusiano mzuri (Mhola)Dagashida waliendesha mkutano vizuri.
Ndipo tulipooona dhahiri kuwa wahenga hawakukosea waliposema tunza mazingira nawe ya kutunze ni usemi uliokuweko toka enzi za mababu zetu sungusungu hawa waliweza kutunza mzingira yao kwa vitendo .
Toka jadi wao ndio walikuwa walinzi wa misitu ya asili hawakuishia hapo walikuwa wanalinda kisima kisichafuliwe kwa kutunza misitu ulio karibu na kisima ili kiwe na maji mengi .
sungusungu walianzisha na kuyatunza maeneo mengine ya kulishia mifugo maarufu kama ngitili hao ndio walikuwa walinzi wakuu mfano mzuri katika vijiji vya Ikonda,Busongo,Mwamishani wanataratibu zao za kutunza ngitili kwa kufanya hivyo waliweza kupunguza kulishia mifugo eneo bila ya ruhusa ya mwenye eneo hilo ukikutwa walikuwa wanakuadhibu kisheria .

Pia waliweza kutatua migogoro ya mipaka ya mashamba katika eneo lao hii ilisaidia katika jamii za kisukuma kuishi kwa amani na upendo .Sungusungu wapo katika kamati za mazingira hivyo hutoa mawazo mazuri katika utunzaji wa misitu ya asili na wao ndio watekelezaji wakuu wa suala zima la utunzaji wa mazingira.
Kuwinda ,kuchunga na kukata miti kulikatazwa kulifanywa kwa ruhusa maalum kutoka kwa mwenyekiti wa sungusungu ukikutwa unalipa faini hii ilisaidia sana jamii ya kisukuma kuweza kuwa na mazingira yaliyoboreshwa kiukamilifu.
Nilikuwa na kiu ya kujua asili hasa ya sungusungu ni nini ndipo hapo bwana mwenyekiti wa sungusungu wa Lubaga aliponielezea sungusungu ilianzishwa mwaka 1982 katika kijiji cha ng’wang’halanga wilayani Nzega. Mzee Mwanamabonde alianzishwa sungusungu baada ya kukutwa na watu walokuwa wameibiwa ng’ombe.
Basi Mwanamabonde akiwa mwenyekiti wa kijiji hicho aliwaambia kuwa pamoja na ng’ombe kuwa wako kwa bwana Pandasahani, itakuwa ni vigumu au haitawezekana ng’ombe hao muwachukue hivi hivi tu.

Mzee Mwanamabonde akawaambia tulieni hapa kwanza. Basi Mwanamabonde akaitisha mkutano wa wanakijiji wake kisha wakaenda pamoja nao kwenye mji wa Pandasahani ambapo ng’ombe mbalimbali wa wizi walitunzwa hapo.

Ilikuwa ni siku Pandasahani alikuwa ameamua kufanya karamu kwani walikuta ng’ombe amechinjwa, nyama zikipikwa jikoni. Jamii iliyochoshwa na vitendo vichafu vya Pandasahani iliwaamuru wake zake Pandasahani kujitwisha vyungu vya nyama kutoka jikoni bila kujali wanaungua kiasi gani. Pandasahani aliambiwa wanapelekwa kituo cha Polisi. Wakiwa pamoja na Pandasahani na familia yote, waliongozwa hadi katikati ya pori ambako waliambiwa kuwa hapa ndiyo kituo cha Polisi.

Waliamuriwa kusali mara ya mwisho kwani siku zao zilikuwa zimekwisha. Sahani na familia yake yote kila mtu kwa wakati wake alisali. Utesaji ulipoanza kwa akina mama kwa kukatwa ziwa moja huku wakiwa hai bado. Hatimaye akina baba nao walionja joto ya jiwe kwa kukatwa sehemu za siri wakiwa hai. Kazi ya mwisho ilikuwa kuuwawa kwa familia ya Pandasahani. Maiti zao ziliachwa porini.
Baada ya kubainika mauaji haya, polisi walikuja, lakini mzee Mwanamabonde alikana akasema hajui kwani halikuwa eneo lake. Polisi wakamwacha huru.

Mzee Mwanamabonde akazuru Kahama kueneza mbinu za kuanzisha Sungunsungu. Akiwa wilayani Kahama, alikutana na mzee Kishosha, mzee Jugi na wengine walioonekana wazuri na maarufu. Aliwaelezea azma yake ya kuanzisha sungusungu. Aliwapa mbinu aliyokuwa akitumia huko kwake.

Harakati hizi za kuanzisha sungusungu zilizagaa na kutafsiriwa kuwa wanaanzisha chama cha siasa. Mkuu wa wilaya Kahama alimwarifu Rais kuwa kuna chama cha siasa kimeanzishwa Kahama. Rais aliagiza mara moja watu hao wafunguliwe na mashitaka. Kweli muda mrefu haukupita watu hawa akina mzee Jugi, mzee Kishosha na wengine wakahukumiwa kifungo cha miezi kumi kila mmoja.

Tume iliteuliwa baadaye walifanyia uchunguzi chama hiki. Katika Tume hiyo akiwemo Mbunge wa Maswa Mheshimiwa Shillingi na wengine. Katika kuwahoji wazee hao waliokuwa wakituhumiwa, Mheshimiwa Shillingi aliwataka waongee kisukuma. Wazee hawa kila mmoja alidai wamechoshwa na wezi. Hapakujitokeza suala la kisiasa hata kidogo.

Tume ikawasilisha taarifa yake kwa Mheshimiwa Rais, muda si mrefu Rais akamuru watu hao waachiliwe mara moja na waendelee kuunda sungusungu yao kwa minajili ya ulinzi wa ng’ombe wao na mali zao nyingine. Katika eneo la Lubaga sungusungu wamefanikiwa kwa kiasi kikiubwa katika utendaji wao wa kazi za kila siku na kusaidia watu kuishi katika amani na usalama.chombo bila nahodha huenda mrama ndivyo inavyokuwa sungusungu wa Lubaga wao kama wao wana utawala wao.
Hakika jeshi la jadi halikuwa na mzaha hata kidogo kwani katika utawala wake kulikuwa na Mtemi (Ntemi) ambaye alichaguliwa kwa kigezo cha kuwa na maarifa ya tiba za jadi au za asili ,na huacha madaraka kwa muda wa miaka mitatu labda aumwe,afe,ahame ndio amejivua uongozi na uongozi haufuati ukoo fulani bali huchaguliwa na wananchi wenyewe.msaidizi wake aliyeitwa Mwambilija “Mtwale”,katibu wake aliitwa mwandiki na msaidizi wake pia kuna kamamanda mkuu aliyetwa kwa jina la asili la Nsumba ntale na wajumbe wa kamati.Katika uongozi wao hawana kiongozi mwanamke kwa minajili ya kwamba wanawake hawawezi kutunza siri lakini kwa uchunguzi tulioufanya kuna matawi mengine kuna wenyeviti wanawake mfano mzuri ni katika kijiji cha Mwagala.
Katika jamii ya wasukuma kuna kuwa na penga mbili (filimbi)viongozi wa familia wanakuwa nazo yaani mama na baba popote wakitokewa na tatizo wanapiga sungusungu na watu wengine wanakuja na katibu anaandika tatizo lililotokea .
“Ndulilu”ni kipande cha kibuyu kilichotobolewa katika sehemu tatu na sehemu mbili zinazibwa sehemu moja inatumika kwa kupiga endapo tu kuna tatizo kubwa mfano wizi wa mifugo na mauwaji.
Tukumbuke kuwa ulinzi wa jadi ni sheria ndogondogo tuliojiwekea ili kujilinda na mali zetu .Endapo mtu ameenda kinyume na sheria tuliojiwekea hupewa adhabu maarufu kama kupigwa “mchenya”ambazo ni faini ndogo ndogo na ukiendelea wanakutenga (kumtulija)ina maana usishiriki katika shughuli zote za jamii ukifiwa watu wanakuja kuzika lakini sungusungu wanawafukuza ndugu zako kuwafariji na kulala matangani na ukifa utakuwa umeikomboa jamii yako.Ukiwa mjeuri,mwizi,unaharibu mazingira kwa kiasi kikubwa unapelekwa kujikomboa katika jeshi jingine na unatozwa faini kubwa Na adhabu zao haziangalii jinsi wala umri.
Kila kwenye mafanikio hakukosi kuwa na matatizo ndivyo ilivyo kwa wenzetu hawa sungusungu hawana vifaa vya ulinzi vya kisasa ,isitoshe kuna watu ambao hukutwa nyakati za usiku lakini si wezi na kwa upande wao yaani sungusungu wenyewe wanakuwa wanakiuka miiko yao kwa kuwa wanafiki na wenye majungu hivyo kukwamisha zoezi zima la ulinzi .
Licha ya hayo kuna mafanikio ambayo wameyapata ni kupungua kwa wimbi la wizi wa mifugo kwani vijana ndio hasa wenye ari na wito wa kulinda nchi yao na mali zao.
Sungusungu wanautaratibu wa usambazaji wa taarifa kwenda tawi jingine ujulikanao kama mwano ni taarifa ya hatari kutoka tawi moja kwenda jingine endapo kuna tatizo limetokea ili waweze kusaidiana kulitatua .Endapo mifugo imepatikana katika tawi jirani huwaarifu na kwenda kuchukua ,au wezi wamepatikana n.k.
Ikiwa mali imepatikana Mwenyewe asipopatikana kwa upande wa mifugo inatunzwa na kutangazwa kwenye matawi ya jirani baada ya miezi sita inakuwa ni mali ya sungusungu na fedha inayopatikana kutokana na faini au mifugo iliyookotwa hupelekwa katika ujenzi wa maendeleo kama vile shule na hospitali.
Kwa hali ilivyo sasa hivi kila mti una mwenyewe ukikutwa umekata mti unapelekwa kwa sungusungu na sungusungu wanakuhukumu.
Kwa upande wangu naona sungusungu ni wazuri katika suala zima la utunzaji wa mazingira hivyo basi sisi wananchi inabidi tuwaunge mkono sungusungu na kwa upande wao basi walegeze adhabu kwa aliyetengwa angalau aweze kushiriki katika masuala ya kidini tofauti na ilivyo sasa.

Serikali kutambua fursa hii iliyopo ya ulinzi wa jadi(sungusungu) ikizingatia suala la ulinzi shirikishi ambao umeonyesha mafanikio makubwa kwa taifa hili hususani vyombo vya ulinzi kwani jamii inachukua nafasi kubwa kama chanzo cha habari.
Mafunzo kwa taasisi za namna hii ni muhimu sana ili kuongeza ufanisi zaidi kwa kuzingatia ukweli na uwazi.

No comments: