Monday, December 29, 2008

HABARI NJEM A KWA WAFUGAJI?

HABARI NJEM A KWA WAFUGAJI?
Na.Mwantumu Jongo.
Suala la matumizi ya madume bora ya ng’ombe ni kitu cha lazima kwa wafugaji wa ng’ombe wa asili, kama wanahitaji kujinasua katika umasikini. Wafugaji wa ng’ombe wa asili, wanatakiwa kuboresha mifugo yao ili iweze kufikia viwango vya kimataifa. Viwango hivyo ni pamoja na kuwa na umbo la kuridhisha na uzito mkubwa, ukilinganishwa na ng’ombe wa sasa wenye maumbo madogo na uzito usiokidhi soko hilo la kimataifa. Kituo cha Taifa cha Madume Bora ya Mbegu za Ng’ombe (NAIC) cha Usa River, Arusha, kina jumla ya madume 25 kwa sasa. Madume hayo ni kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora za ng’ombe wa maziwa na nyama. Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, imeanza kuchukua hatua kadhaa ili kuwakomboa wafugaji wa ng’ombe wa asili katika ushindani wa soko la kimataifa. Moja ya hatua hizo ni kutoa huduma ya mbegu bora za madume, ambayo itaweza kuwatoa katika aina duni ya ng’ombe wanaomiliki hivi sasa. Hivi karibuni nilitembelea kituo hicho cha madume bora. Kituo hicho hakifahamiki sana na wafugaji wa ng’ombe wa asili. Wafugaji wengi niliowahoji walisema hawatambui kuwapo kwa kituo hicho muhimu kwao katika kufanya mageuzi ya kibiashara hatua kwa hatua. Wachache walisema wanadhani kituo hicho kinajishughulisha na uzalishaji wa mbegu bora, kwa ajili ya ng’ombe bora wa maziwa. Kwa kifupi, Kituo cha Mbegu Bora cha Taifa (NAIC) kina ukubwa wa eka 315, ambapo eka 45 kati ya hizo, zinamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru, kwa ajili ya upanuzi wa mji wa Usa River. Eka 50 ni msitu wa asili, eka 40 ni majengo, eka 53 ni eneo la maabara, eka 27 ni miamba na eka 135 ni maeneo ya kulima majani kwa ajili ya madume yanayofugwa hapo. Kituo kina uwezo wa kutunza madume 88 na mahitaji ya malisho ni eka 2.5 kwa dume moja. Hivyo madume 88 yanahitaji eka 170. Madhumuni ya kuanzisha kituo hicho ni kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama ili kuinua pato la Taifa na la wafugaji na kuboresha lishe nchini. Kuzalisha mifugo kwa njia ya uhamilishaji, kunasaidia kuzuia gharama zisizo za lazima, kutunza madume na kuepukana na hatari ya kujeruhiwa na madume au dume kujeruhi ng’ombe wenzake. Njia hii pia inasaidia kuzuia kuenea kwa magonjwa ya vizazi na kusafirisha mbegu bora kirahisi kutoka eneo moja hadi jingine. Njia ya uhamilishaji pia inafanya mfugaji apate ndama wengi, kutokana na dume moja kwa muda mfupi kwa sababu dozi 200 na zaidi za mbegu, zinaweza kukusanywa kwa siku moja kutoka kwenye dume moja. Kwa njia ya asili dume moja hupanda majike 30 kwa mwaka. Mbegu za dume zinaweza kuvunwa leo na kukaa muda mrefu, hata kama dume huyo atakuwa amevunjika au kufa, kwa sababu mbegu zake zinahifadhiwa na kutunzwa kwa muda wa miaka 20 na zaidi zikiwa hai. Vile vile inasaidia mfugaji kuwa na wigo mpana kuchagua aina ya mbegu anayohitaji. Pamoja na kuzalisha mbegu bora za madume, NAIC kinazalisha hewa baridi ya nitrojeni, kwa ajili ya kuhifadhia mbegu. Bila hewa hiyo huwezi kuhifadhi mbegu hizo, hii ni pamoja na kutoa vifaa vya uhamilishaji, ambavyo ni mitungi ya kuhifadhia na kusafirisha mbegu, bunduki na mirija ya kupandishia ngombe na glovu za kuvaa mikononi. Pia NAIC kinafundisha wataalamu wa uhamilishaji, ikiwa ni pamoja na watu binafsi na wataalamu wanaoteuliwa na vikundi vya wafugaji. Vile vile hutoa mafunzo na taarifa muhimu kuhusu ufugaji kwa vikundi vya wafugaji na wakulima, kutunza kumbukumbu za uhamilishaji, kupima mimba changa kwa kutumia maziwa. Kwa sasa kituo kina madume 25 ya aina za Ayrshire madume tisa Fresian, madume matano Jersey. Aina hizo tatu za madume ni kwa ajili ya maziwa. Aina nyingine ya madume matano ya Sahiwal na madume manne aina ya Mpwapwa. Aina hizo mbili za madume ni kwa ajili ya maziwa na nyama. Aina ya mwisho ya madume ni madume aina ya Boran, ambayo yapo matatu. Aina hii ni kwa ajili ya nyama. Kwa sasa sehemu kubwa ya mbegu za ng’ombe wa nyama, zinatumika kwenye mashamba ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). Hivyo basi, wafugaji wa asili wanaofuga karibu na ranchi za taifa wanayo nafasi kubwa ya kujiweka katika vikundi na kuomba kupata elimu na gharama za uhamilishaji kutoka katika ranchi. Hii itakuwa ni nafasi nzuri kwao kuanza kupata huduma ya uhamilishaji na kubadilisha ubora wa uzao utakaozaliwa kwenye mifugo yao. Madume aina ya Sahiwal ni mazuri kuhamilisha kwa ng’ombe wa asili ili kuweza kupata ng’ombe wenye nyama nyingi watakaokidhi soko la nje. Dume aina ya Sahiwal ni maarufu kwa ajili ya nyama na maziwa. Dume huyo ana kawaida ya kuzaa watoto wenye sifa ya kutoa maziwa na ukuaji wa haraka. Asili ya dume huyo ni Nakuru, Kenya. Aina hiyo ya ng’ombe inafaa sana kwa wafugaji wa mikoa ya Shinyanga, Arusha na Dodoma. Wanahimili magonjwa na ukame, wanakua haraka sana na wana umbo kubwa lenye nyama. Dume aina ya Boran anaongeza nyama kwa ng’ombe wa asili. Wafugaji nchini wanaweza kutumia aina hiyo ya madume katika shughuli zao za ufugaji, kutokana na ukweli kwamba aina hiyo ya madume huwezesha kupatikana aina nzuri ya ng’ombe wa nyama na maziwa. Hatua hiyo inaweza kuwasaidia kujiongezea pato lao na la Taifa kwa ujumla.

No comments: