Tuesday, December 30, 2008

ATHARI ZIPI HUPATIKANA KWA KUTOMNYONYESHA MTOTO
Wakinamama wa kisasa wameibua tabia ya kutotaka kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama kwa kuhofia kupoteza uhalisia wa matiti yao eti kwa kile kinachoitwa kulegea na hivyo kupoteza umbo lake la awali.Hali hii imekuwa ikienea kwa kasi katika jamii nyingi na kuchangia kasi ya ongezeko la vifo vya watoto wachanga na watoto kuanzia umri wa miaka miwili hadi mitano.

Ingawa hata wale wanawake wengi wanaonyonyesha , hawanyonyeshi inavyotakiwa hali hii inatokana na sababu nyingi kwa mfano desturi ya kulikiza mapema ,kukosa
wa kunyonyesha kwa sababu ya kazi nyingi na fikra potofu zinazowafanya wanawake wasinyonyeshe kama vile kuamini mama akiwa mjamzito asinyonyeshe au mtoto akiharisha hatakiwi kunyonyeshwa.


Kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama ni muhimu sana kwa afya bora na ukuaji wake hii inatokana kwamba maziwa ya mama ni chakula kilicho salama na chenye virutubisho vyote ubora wa maziwa ya mama kwa mtoto anapozaliwa hadi kufikia miezi minne chakula chake kikuu ni maziwa ya mama maziwa hayo ndio chakula ambacho pekee bora ambacho mtoto anaweza kupewa.

Ubora wa maziwa ya mama unatokana na maziwa ya mama kuwa ndio mlo pekee salama na wenye virutubisho vyote ,maziwa ya mama yanasaidia kumkinga mtoto asipate magonjwa kama vile kuharisha ,kifua na surua.Maziwa ya mama ni rahisi hayana gharama na yako tayari kwa wakati wowote na isitoshe yana maji ya kutosha kwa mahitaji ya mtoto.

Mama huanza kunyonyesha mtoto mara tu baada ya kuzaliwa maziwa ya mwanzo ni muhimu sana kwasababu yana virutubisho na viini vya kinga ya asili kwa magonjwa na wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa maziwa haya yasikamuliwe na kumwagwa kama watu wengine wanavyofikiria kuwa maziwa haya yana madhara kutokana na rangi yake.

Mtoto baada ya kuzaliwa anyonyweshe maziwa asipewe kinywaji cha aina yeyote ,anyonyeshwe maziwa ya mama tu mpaka atakapofikia miezi minne. Wakati wa kunyonyesha mama anatakiwa kuzingatia mambo mengine muhimu anawe mikono na kuosha matiti kabla ya kumnyonyesha mtoto ,anyonyeshe akiwa amekaa ametulia ,amwekee mtoto chuchu yote mdomoni na kumshikiria titi .Kila wakati mama anaponyonyesha mtoto anyonyeshe matiti yote mawili,amnyonyeshe mtoto mpaka ashibe kabisa,amtoe mtoto hewa kwa kumweka begani na kumsugua taratibu mara baadaya kunyonya.

Kunyonyesha maziwa ya mama kuna faida nyingi kwa mtoto na hata kwa mama mwenyewe kwani kunasababisha maziwa ya mama kutoka hivyo kumwezesha mtoto kuendelea kunyonya na kushiba vizuri,humkinga dhidi ya magonjwa mengi ya hatari,humsaidia mama asipate ujauzito endapo mama hatakuwa anapata siku zake za hedhi hasa katika kipindi cha miezi sita toka ajifungue , kunyonyesha kunazuia matiti kujaa na kuuma ,hurudisha viungo vya uzazi katika hali yake ya kawaida

Matatizo yanayoweza kusababisha mtoto asinyonye vizuri ni pamoja na mtoto kutopakatwa vizuri,chuchu za mama zikiwa na vidonda au fupi na hata kuzimeziba , mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati wake (njiti),mtoto mwenye kilema cha mdomo na lishe duni kwa mama hivyo maziwa hayatoshi.

Tatizo hili huwakuta wakinamama wanaojifungua kwa mara ya kwanza kinachotakiwa mama azivute chuchu mara kwa mara hadi zitakapotoka kiasi cha kutosha kwa upande wa mtoto njiti au mwenye kilema anatakiwa mama amkamulie maziwa kwenye chombo na amnyonyeshe mtoto.Kwa mama mwenye chuchu zenye vidonda asafishe chuchu na amkamulie na ahakikishe kuwa anasafisha chuchu mara kwa mara.

Wajibu wa serikali ni kuandaa na kuratibu shughuli za kuelimisha jamii juu ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwani kunyonyesha maziwa ya mama ni muhimu sana kwa ukuaji na maendeleo ya mtoto .Maisha ya watoto wengi yangeokolewa kama kinamama wangenyonyesha vizuri watoto wao ipasavyo watoto wengi nchini hawanyonyeshwi vizuri kwa sababu nyingi baadhi ya sababu hizo ni kinamama kuelemewa na kazi nyingi na hivyo kukosa muda wa kunyonyesha pia jamii kukosa elimu ya unyonyeshaji na kuwepo kwa baadhi ya mila na destuli zinazoathiri unyonyeshaji .katika kuboresha unyonyeshaji juhudi zaidi ziwekwe katika sababu zinazowafanya wakinamama wasinyonyeshe.

No comments: